Thursday

WANAFUNZI WANASOMA KWA KUGEUZIANA MIGONGO RUVUMA

WANAFUNZI 201 kuanzia darasa la tatu hadi la sita  katika shule ya msingi Kidugalo kata ya Rwinga wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma wanasoma katika vyumba viwili vya madarasa kwa kugeuziana migongo hali ambayo inachangia kushusha taaluma katika shule hiyo.
Wanafunzi wa darasa la tatu na la nne katika shule ya msingi Kidugalo kata ya Rwinga Namtumbo mjini mkoani Ruvuma wakisoma katika chumba kimoja kwa kugeuziana migongo

Mwalimu mkuu wa shule hiyo Owini Mpangala alibainisha kuwa  wanafunzi 51 wa darasa la tatu na wanafunzi 56 wa darasa la nne wanasoma katika chumba kimoja kwa kugeuziana migongo na wanafunzi 62 wa darasa la tano na wanafunzi 32 wa darasa la sita wanasoma katika chumba kimoja kwa kugeuziana migongo.
“Madarasa mawili kusomea katika chumba kimoja kunasababisha kila darasa kufundishwa vipindi vinne tu kati ya vipindi nane vinavyotakiwa kufundishwa kwa siku,walimu wawili hawawezi kuingia kwa wakati mmoja kufundisha kwenye chumba kimoja,vipindi vinne vinapotea  darasa halifundishiki’’,alisisitiza.
Kwa mujibu wa mwalimu Mpangala shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 2007 yenye wanafunzi 453 ina vyumba vinne tu vya madarasa kati ya mahitaji ya vyumba nane na kwamba shule hiyo haina ofisi ya walimu hali ambayo inasababisha mwalimu mkuu na walimu kutumia ofisi moja ambayo hata hivyo haitoshi kutokana na idadi ya walimu 13 waliopo katika shule hiyo.
Kutokana na hali hiyo baadhi ya walimu wanakaa nje ya ofisi wakati wa kiangazi huku wakiendelea kufanyakazi za kusahihisha madaftari ya wanafunzi wakipigwa na jua hali ambayo inaleta kero kubwa kwa walimu na wanafunzi.
Mkuu wa shule hiyo alisema amechukua hatua mbalimbali za kukabiliana na matatizo hayo ikiwa ni pamoja na kuyapeleka katika kamati ya shule na Baraza la madiwani ambayo wameahidi katika msimu ujao wa fedha wanatarajia kulipatia kipaumbele hasa kero ya upungufu wa vyumba vya madarasa,samani na ofisi ya walimu.
“Hapa kwangu uongozi wa serikali ya kijiji umekataa kujenga vibanda vya nyasi kama ilivyo katika shule nyingine kwa madai kuwa hapa ni mjini hawawezi kujenga vibanda vya nyasi ni aibu,wamefyatua tofali zipo kwenye tanuri’’,alisema.
Baadhi ya walimu wanaofundisha katika shule hiyo wamesema wanatamani kuacha kazi au kuhama katika shule hiyo kutokana na changamoto nyingi ambazo hazijapatiwa ufumbuzi kwa muda mrefu na kuchangia kushusha elimu katika shule hiyo ambayo ipo mjini.
Mratibu elimu kata ya Rwinga Thomas Komba amekiri shule za msingi katika kata yake inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo shule ya msingi Kidugalo ambapo hivi sasa uhamasishaji unafanyika ili kumaliza kero ya upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa.
Baadhi ya walimu katika shule ya msingi Kidugalo wakisahihisha madaftari ya wanafunzi nje baada ya shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 2007 kukosa ofisi ya walimu

Aliongeza kuwa wananchi wa eneo la Kidugalo mwaka jana wamefyatua na kuchoma tofali kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na kwamba hivi sasa kinachosubiriwa ni nguvu toka serikalini kutoa vifaa vya kiwandani ili kuweza kufanikisha kupunguza kero hiyo ya muda mrefu.
Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo ina shule za msingi 107 kati ya hizo shule 105 zinamilikiwa na serikali na shule mbili ni za watu binafsi na mashirika ya dini.
Imeandaliwa na Albano Midelo,Namtumbo

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.

Search This Blog