On Streets Today
Msanii AT kutoka Zanzibar akitumbuiza jukwaani na wacheza shoo wake wakati wa onyesho maalum la Washindi wa Kili Music Awards jijini Mbeya kwenye Uwanja wa Sokoine juzi. (Picha: Mpigapicha Wetu) |
Nyota
wa hip hop nchini, Roma Mkatoliki, aliacha gumzo mjini Mbeya wakati
alipofanya shoo ya uhakika na kuamsha shangwe mpya, licha ya kuwa
msanii wa pili kutoka mwisho katika ratiba ya watumbuizaji wa onyesho
la ziara ya washindi wa tuzo za Kilimanjaro kwenye Uwanja wa Sokoine
juzi.
Mashabiki waliimba jina lake tangu msanii huyo alipoitwa stejini na alipofika hakuwaangusha.
Alitumbuiza
kwa nyimbo zake kali na wakati mashabiki wakidhani kwamba shoo yake
imefikia tamati, rapa huyo alisema: "Sasa ndugu zangu, nawaambia ukweli
kwamba kufikia muda huu mmetumia Sh. 200 tu ya kiingilio chenu... sasa
nawapa shoo ya Sh. 1,800 iliyobaki.”
Huku mashabiki wakishangilia kwa nguvu, Roma alimalizia kwa kuimba wimbo wa Mathematic uliompa tuzo.
Wasanii
wengine waliopanda stejini ni pamoja na Ben Pol, AT, Ali Kiba, Barnaba,
Ommy Dimpoz na Suma Lee ambao nao walifanya shoo ya uhakika.
Mshindi
wa tuzo ya wimbo bora wa R&B, Ben Paul ambaye alijinyakulia tuzo
hiyo kupitia wimbo wake wa 'Number One', alifungua jukwaa na kuwaamsha
watu kuwa sasa shoo imeanza.
Alifuata
jukwaani Suma Lee ambaye aliongozwa na shoo kali kutoka kwa vijana wake
wanne wa kike na wa kiume na kushangiliwa vilivyo.
Kisha
alipanda mkali kutoka Zanzibar ambaye ni mshindi wa Tuzo Wimbo Bora
wenye Vionjo vya Kiasili, Ally Tall a.k.a AT na kutoa burudani ya nguvu
na wimbo wa 'Vifuu Tundu' akiwa na wanenguaji wake wawili wa kike.
Nyota
wa wimbo 'Baadaye', Ommy Dimpoz alipanda jukwaani na kutumbuiza kwa
wimbo huo pamoja na 'Nai Nai' uliompa tuzo ya Wimbo Bora wa
Kushirikiana aliomshirikisha Ali Kiba.
Ali
Kiba alibaki jukwaani hapo kama ilivyokuwa mjini Moshi na vijana wake
kumfuata kutoa shukrani zao za kupata kura zilizowapa ushindi wa tuzo
ya Wimbo Bora wa Zouk Rhumba kupitia wimbo wa 'Dushelele'.
Mshindi
wa Tuzo ya Mwimbaji Bora wa Kiume, Barnaba ndiye aliyefunga pazia hilo
mjini Mbeya kwa kuimba wimbo wake unaotamba sasa wa 'Magube Gube'.
Wasanii
hao wiki ijayo wanataraji kutoa burudani kama hiyo jijini Mjini Mtwara,
baada ya kuwa tayari walishatumbuizakatika miji ya Dodoma, Mwanza na
Moshi.