WANAFUNZI 201 kuanzia darasa la tatu hadi la sita katika shule ya
msingi Kidugalo kata ya Rwinga wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma wanasoma
katika vyumba viwili vya madarasa kwa kugeuziana migongo hali ambayo
inachangia kushusha taaluma katika shule hiyo.
|
Wanafunzi
wa darasa la tatu na la nne katika shule ya msingi Kidugalo kata ya
Rwinga Namtumbo mjini mkoani Ruvuma wakisoma katika chumba kimoja kwa
kugeuziana migongo |
Mwalimu mkuu wa shule hiyo Owini Mpangala alibainisha kuwa wanafunzi
51 wa darasa la tatu na wanafunzi 56 wa darasa la nne wanasoma katika
chumba kimoja kwa kugeuziana migongo na wanafunzi 62 wa darasa la tano
na wanafunzi 32 wa darasa la sita wanasoma katika chumba kimoja kwa
kugeuziana migongo.
“Madarasa mawili kusomea katika chumba kimoja kunasababisha kila
darasa kufundishwa vipindi vinne tu kati ya vipindi nane vinavyotakiwa
kufundishwa kwa siku,walimu wawili hawawezi kuingia kwa wakati mmoja
kufundisha kwenye chumba kimoja,vipindi vinne vinapotea darasa
halifundishiki’’,alisisitiza.
Kwa mujibu wa mwalimu Mpangala shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 2007
yenye wanafunzi 453 ina vyumba vinne tu vya madarasa kati ya mahitaji ya
vyumba nane na kwamba shule hiyo haina ofisi ya walimu hali ambayo
inasababisha mwalimu mkuu na walimu kutumia ofisi moja ambayo hata hivyo
haitoshi kutokana na idadi ya walimu 13 waliopo katika shule hiyo.
Kutokana na hali hiyo baadhi ya walimu wanakaa nje ya ofisi wakati wa
kiangazi huku wakiendelea kufanyakazi za kusahihisha madaftari ya
wanafunzi wakipigwa na jua hali ambayo inaleta kero kubwa kwa walimu na
wanafunzi.
Mkuu wa shule hiyo alisema amechukua hatua mbalimbali za kukabiliana
na matatizo hayo ikiwa ni pamoja na kuyapeleka katika kamati ya shule na
Baraza la madiwani ambayo wameahidi katika msimu ujao wa fedha
wanatarajia kulipatia kipaumbele hasa kero ya upungufu wa vyumba vya
madarasa,samani na ofisi ya walimu.
“Hapa kwangu uongozi wa serikali ya kijiji umekataa kujenga vibanda
vya nyasi kama ilivyo katika shule nyingine kwa madai kuwa hapa ni mjini
hawawezi kujenga vibanda vya nyasi ni aibu,wamefyatua tofali zipo
kwenye tanuri’’,alisema.
Baadhi ya walimu wanaofundisha katika shule hiyo wamesema wanatamani
kuacha kazi au kuhama katika shule hiyo kutokana na changamoto nyingi
ambazo hazijapatiwa ufumbuzi kwa muda mrefu na kuchangia kushusha elimu
katika shule hiyo ambayo ipo mjini.
Mratibu elimu kata ya Rwinga Thomas Komba amekiri shule za msingi
katika kata yake inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo shule ya
msingi Kidugalo ambapo hivi sasa uhamasishaji unafanyika ili kumaliza
kero ya upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa.
|
Baadhi
ya walimu katika shule ya msingi Kidugalo wakisahihisha madaftari ya
wanafunzi nje baada ya shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 2007 kukosa ofisi
ya walimu |
Aliongeza kuwa wananchi wa eneo la Kidugalo mwaka jana wamefyatua na
kuchoma tofali kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na kwamba hivi
sasa kinachosubiriwa ni nguvu toka serikalini kutoa vifaa vya kiwandani
ili kuweza kufanikisha kupunguza kero hiyo ya muda mrefu.
Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo ina shule za msingi 107 kati ya
hizo shule 105 zinamilikiwa na serikali na shule mbili ni za watu
binafsi na mashirika ya dini.
Imeandaliwa na Albano Midelo,Namtumbo