Tuesday

Naibu Spika wa Bunge wa zamani afariki dunia

On Streets Today

Naibu Spika wa Bunge wa zamani, Mathias Michael Kihaule, amefariki dunia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), jijini Dar es Salaam, alikokuwa amelazwa.

Kwa mujibu wa taarifa Idara ya Habari, Elimu kwa Umma na Ushirikiano wa Kimataifa, Ofisi ya Bunge, jijini Dar es Salaam iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana, alifariki Jumapili ya Mei 3, mwaka huu.

Kihaule ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Ludewa, mkoani Iringa, alizaliwa Julai 19, 1933 na amefariki akiwa na umri wa miaka 79.

Licha ya kuwa mbunge wa jimbo hilo kwa kipindi cha miaka 15, kuanzia mwaka 1980-1995, Kihaule alilitumikia taifa katika wadhifa wa Naibu Spika wa Bunge.

Alikuwa na wadhifa huo katika kipindi chake cha tatu cha ubunge, kuanzia mwaka 1990 mpaka mwaka 1995.

Baada ya kipindi chake cha ubunge, aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, mkoani Mbeya, kuanzia mwaka 1995 hadi 2004.

Katika utumishi wake wa umma, Kihaule amewahi pia kushika nyadhifa kadhaa kitaaluma, ikiwamo Mkufunzi wa Vyuo mbalimbali vya Ualimu nchini.

Hadi alipofariki, alikuwa akijihusisha na shughuli mbalimbali za kilimo na ufugaji, na atakumbukwa na wananchi wa Ludewa kwa jinsi alivyokuwa akishirikiana nao katika  maendeleo ya jimbo na wilaya yake kwa kipindi chote alichokuwa bungeni na mara baada ya kumaliza muda wake wa ubunge.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mipango ya mazishi inafanywa nyumbani kwa mtoto wake, Dk Anold Kihaule, Ilala Maghorofani, ambako ibada ya kuaga mwili itafanyika leo Msimbazi Centre kuanzia saa 6 mchana, kabla ya kusafirishwa kesho kwa ndege kwenda Ludewa kwa mazishi.
Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahala pema peponi. Amin.
CHANZO: NIPASHE

Siri nzito yafichuka Chadema

On Streets Today

                   
                        Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe
 
Maandamano na mikutano ya hadhara inayofanywa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), imebainika kuwa ni sehemu ya mikakati yake inayolenga kuibua chuki za wananchi na kukiangusha Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Vyanzo vya habari ndani vya Chadema ambavyo havikutaka kutajwa majina yao, vimelieleza NIPASHE Jumapili kuwa, chama hicho kilifanya tathmini na kubaini kasoro zilizochangia kushindwa katika Uchaguzi Mkuu wa 2010.
Miongoni mwa kasoro hizo, ni ari ndogo iliyojitokeza kwa wananchi kulinda kura za wagombea urais na ubunge kupitia Chadema.
“Ili wananchi wawe tayari kuona umuhimu wa kulinda kura za chama cha siasa, inabidi wawachukie watawala, sasa tunachokifanya ni kueleza upungufu wa chama tawala ili wananchi waamke, waichukie CCM,” kilieleza chanzo hicho.
Hata hivyo, akihutubia mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa Mahakama jana, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, pamoja na mambo mengine alisema chama hicho kitaendelea kuwachochea wananchi kuiasi CCM na kukiunga mkono chama chake.
Mbowe alisema, “wanasema Mbowe ni mchochezi, wanasema Chadema inapandikiza chuki, mimi na chama changu tutaendelea kuuhamasisha umma kuondokana na woga, wawachukie watawala walioshindwa kuwaletea maendeleo.”
Chadema imekuwa na utaratibu wa kuandaa maandamano na mikutano ya hadhara kupitia kile kinachojulikana kama operesheni maalum, mathalani kwa sasa ikijulikana kama Operesheni Okoa Kusini.
KUCHUKUA MFUMO WA CCM
Kwa upande mwingine, mkakati uliobuniwa na kuzinduliwa na Chadema, ukijulikana kama Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) umetajwa kama wenye lengo la kukisimika chama hicho hadi kwenye ngazi ya ubalozi, kama ilivyo kwa CCM.
Kupitia M4C Chadema inajikita kwa ‘kuvuna’ wanachama na kusimika uongozi katika ngazi tofauti kuanzia mabalozi, matawi, kata, jimbo, wilaya, mkoa hatimaye taifa.
Tayari Chadema kwa kutambua umuhimu wa kukiweka chama katika ngazi ya msingi (ubalozi), kimetumia ibara ya 7.1.1 ya Katiba yake kimeweka tarehe ya kufanyika uchaguzi nchi nzima.
Mbali na ngazi ya ubalozi, Chadema imetumia ibara ya 7.1.3 kutangaza uchaguzi wa chama hicho ngazi ya tawi, ambapo awali kilionekana kutokuwepo katika maeneo mengi ya nchi.
“Tunapoingia ndani ya jamii kufikia ngazi za msingi, tawi na kata, tutajihakikishia kuichukua nchi kwa urahisi zaidi,” kilieleza chanzo hicho.
Chadema imetoa maelezo ya taratibu za uendeshaji wa uchaguzi ndani ya chama hicho kwa ngazi za msingi na matawi, kikitumia ibara ya 11-1 ya chama hicho na kuzisambaza nchi nzima.
Mkurugenzi wa Kampeni na Uchaguzi wa Chadema, Msafiri Mtemelwa, alithibitisha kuchapishwa kwa maelezo hayo na kwamba yatafanikisha chaguzi hizo kufanyika kwa mujibu wa Katiba.
Maelezo hayo yanataja Septemba Mosi hadi Oktoba 5, mwaka huu kuwa siku za uchaguzi ngazi za msingi wakati ule wa matawi utafanyika kati ya Desemba 5 hadi Januari 8, mwaka ujao.
Chaguzi nyingine na ngazi zake kwenye mabano zitafanyika Februari 8 hadi Machi 14, mwaka ujao (kata), Aprili 14 hadi Mei 23, mwaka ujao (jimbo), Juni 23 hadi Julai Mosi, 2013 (wilaya) na Agosti 2 hadi Septemba 11 mwakani (mkoa).
Chaguzi zote hizo zitafanyika zikihusisha pia mabaraza tofauti ya Chadema, lile la vijana (Bavicha), wanawake (Bawacha) na Wazee.
Chanzo kimeeleza kuwa kupatikana kwa uongozi katika ngazi hizo kutaiwezesha Chadema kuwa na mtandao utakaohusika katika kulinda nafasi za wagombea uwenyekiti wa mitaa, vitongoji na vijiji, udiwani, ubunge na urais.
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Mwembe Mmoja (CCM) mkoani Mtwara , Abdallah Suleiman Mnyalu, alisema kazi za kisiasa hususani kukutana na kuzungumza na wananchi, zitaiathiri CCM katika chaguzi zijazo.
Alipotakiwa na NIPASHE Jumapili atoe maoni yake kuhusu athari za Chadema katika ngazi za msingi kwenye jamii, Mnyalu alisema chama hicho kinafanya kazi zilizopaswa kufanywa na CCM, lakini chama hicho tawala kimelala.
“Wenzetu hawa wanapita na kukutana na wananchi, lakini sisi wenye dola hatufanyi hivyo mpaka ufike Uchaguzi Mkuu,” alisema.
Mnyalu alisema pia kuwa vitendo vya unyanyasaji vinavyofanywa na viongozi wa serikali katika ngazi za msingi vimechochea chuki ya wananchi kwa chama tawala, hivyo kutoa mwanya kwa wapinzani hususani Chadema kuungwa mkono.
MATUMIZI YA MTANDAO WA MAWASILIANO
Imebainika kuwa Chadema imejizatiti kutumia njia mbalimbali kuwafikia wapiga kura, wakiwemo wasiojitokeza na kushiriki shughuli za kisiasa hadharani.
Kupitia mkakati huo, imeelezwa kuwa chama hicho kitatumia njia ya mitandao ya kijamii iliyopo kwenye mawasiliano ya kisasa, kupenyeza kampeni na hoja zake.
MKAKATI WA KUJIENEZA
Kikiwa katika Operesheni Okoa Kusini inayoendelea kwenye mikoa ya Lindi na Mtwara, Chadema kinawatumia viongozi na makada wake kufika maeneo ya vitongoji, vijiji na kata ambapo wanazungumza na wananchi, kufungua matawi na kusimika uongozi wa muda.
Jana, Chadema kilichoanza ziara zake mkoani Mtwara Mei 27, mwaka huu, kimeingia mkoani Lindi ambapo kitafanya mikutano ya hadhara na kufungua matawi yake hadi Juni 9, mwaka huu kitakapofanya mkutano wa hadhara mjini Lindi.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

Search This Blog