On Streets Today
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe
Vyanzo vya habari ndani vya Chadema
ambavyo havikutaka kutajwa majina yao, vimelieleza NIPASHE Jumapili
kuwa, chama hicho kilifanya tathmini na kubaini kasoro zilizochangia
kushindwa katika Uchaguzi Mkuu wa 2010.
Miongoni mwa kasoro hizo, ni ari ndogo iliyojitokeza kwa wananchi kulinda kura za wagombea urais na ubunge kupitia Chadema.
“Ili wananchi wawe tayari kuona umuhimu wa
kulinda kura za chama cha siasa, inabidi wawachukie watawala, sasa
tunachokifanya ni kueleza upungufu wa chama tawala ili wananchi waamke,
waichukie CCM,” kilieleza chanzo hicho.
Hata hivyo, akihutubia mkutano wa hadhara
kwenye uwanja wa Mahakama jana, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe,
pamoja na mambo mengine alisema chama hicho kitaendelea kuwachochea
wananchi kuiasi CCM na kukiunga mkono chama chake.
Mbowe alisema, “wanasema Mbowe ni
mchochezi, wanasema Chadema inapandikiza chuki, mimi na chama changu
tutaendelea kuuhamasisha umma kuondokana na woga, wawachukie watawala
walioshindwa kuwaletea maendeleo.”
Chadema imekuwa na utaratibu wa kuandaa
maandamano na mikutano ya hadhara kupitia kile kinachojulikana kama
operesheni maalum, mathalani kwa sasa ikijulikana kama Operesheni Okoa
Kusini.
KUCHUKUA MFUMO WA CCM
Kwa upande mwingine, mkakati uliobuniwa na
kuzinduliwa na Chadema, ukijulikana kama Vuguvugu la Mabadiliko (M4C)
umetajwa kama wenye lengo la kukisimika chama hicho hadi kwenye ngazi ya
ubalozi, kama ilivyo kwa CCM.
Kupitia M4C Chadema inajikita kwa ‘kuvuna’
wanachama na kusimika uongozi katika ngazi tofauti kuanzia mabalozi,
matawi, kata, jimbo, wilaya, mkoa hatimaye taifa.
Tayari Chadema kwa kutambua umuhimu wa
kukiweka chama katika ngazi ya msingi (ubalozi), kimetumia ibara ya
7.1.1 ya Katiba yake kimeweka tarehe ya kufanyika uchaguzi nchi nzima.
Mbali na ngazi ya ubalozi, Chadema
imetumia ibara ya 7.1.3 kutangaza uchaguzi wa chama hicho ngazi ya tawi,
ambapo awali kilionekana kutokuwepo katika maeneo mengi ya nchi.
“Tunapoingia ndani ya jamii kufikia ngazi
za msingi, tawi na kata, tutajihakikishia kuichukua nchi kwa urahisi
zaidi,” kilieleza chanzo hicho.
Chadema imetoa maelezo ya taratibu za
uendeshaji wa uchaguzi ndani ya chama hicho kwa ngazi za msingi na
matawi, kikitumia ibara ya 11-1 ya chama hicho na kuzisambaza nchi
nzima.
Mkurugenzi wa Kampeni na Uchaguzi wa
Chadema, Msafiri Mtemelwa, alithibitisha kuchapishwa kwa maelezo hayo na
kwamba yatafanikisha chaguzi hizo kufanyika kwa mujibu wa Katiba.
Maelezo hayo yanataja Septemba Mosi hadi
Oktoba 5, mwaka huu kuwa siku za uchaguzi ngazi za msingi wakati ule wa
matawi utafanyika kati ya Desemba 5 hadi Januari 8, mwaka ujao.
Chaguzi nyingine na ngazi zake kwenye
mabano zitafanyika Februari 8 hadi Machi 14, mwaka ujao (kata), Aprili
14 hadi Mei 23, mwaka ujao (jimbo), Juni 23 hadi Julai Mosi, 2013
(wilaya) na Agosti 2 hadi Septemba 11 mwakani (mkoa).
Chaguzi zote hizo zitafanyika zikihusisha
pia mabaraza tofauti ya Chadema, lile la vijana (Bavicha), wanawake
(Bawacha) na Wazee.
Chanzo kimeeleza kuwa kupatikana kwa
uongozi katika ngazi hizo kutaiwezesha Chadema kuwa na mtandao
utakaohusika katika kulinda nafasi za wagombea uwenyekiti wa mitaa,
vitongoji na vijiji, udiwani, ubunge na urais.
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha
Mwembe Mmoja (CCM) mkoani Mtwara , Abdallah Suleiman Mnyalu, alisema
kazi za kisiasa hususani kukutana na kuzungumza na wananchi, zitaiathiri
CCM katika chaguzi zijazo.
Alipotakiwa na NIPASHE Jumapili atoe maoni
yake kuhusu athari za Chadema katika ngazi za msingi kwenye jamii,
Mnyalu alisema chama hicho kinafanya kazi zilizopaswa kufanywa na CCM,
lakini chama hicho tawala kimelala.
“Wenzetu hawa wanapita na kukutana na wananchi, lakini sisi wenye dola hatufanyi hivyo mpaka ufike Uchaguzi Mkuu,” alisema.
Mnyalu alisema pia kuwa vitendo vya
unyanyasaji vinavyofanywa na viongozi wa serikali katika ngazi za msingi
vimechochea chuki ya wananchi kwa chama tawala, hivyo kutoa mwanya kwa
wapinzani hususani Chadema kuungwa mkono.
MATUMIZI YA MTANDAO WA MAWASILIANO
Imebainika kuwa Chadema imejizatiti
kutumia njia mbalimbali kuwafikia wapiga kura, wakiwemo wasiojitokeza na
kushiriki shughuli za kisiasa hadharani.
Kupitia mkakati huo, imeelezwa kuwa chama
hicho kitatumia njia ya mitandao ya kijamii iliyopo kwenye mawasiliano
ya kisasa, kupenyeza kampeni na hoja zake.
MKAKATI WA KUJIENEZA
Kikiwa katika Operesheni Okoa Kusini
inayoendelea kwenye mikoa ya Lindi na Mtwara, Chadema kinawatumia
viongozi na makada wake kufika maeneo ya vitongoji, vijiji na kata
ambapo wanazungumza na wananchi, kufungua matawi na kusimika uongozi wa
muda.
Jana, Chadema kilichoanza ziara zake
mkoani Mtwara Mei 27, mwaka huu, kimeingia mkoani Lindi ambapo kitafanya
mikutano ya hadhara na kufungua matawi yake hadi Juni 9, mwaka huu
kitakapofanya mkutano wa hadhara mjini Lindi.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.